Kampeni ya utoaji chanjo ya homa ya mafua makali yaendelea ukanda wa ulaya: WHO
Listen now
Description
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO kanda ya ulaya tangu kuanza kwa msimu wa baridi kali katikati ya mwezi Novemba mwaka 2022 wamebaini kuongezeka kwa wagonjwa wanaolazwa kutokana na magonjwa ya homa ya mafua makali au flu,  matatizo ya kupumua na COVID-19. Walio hatarini zaidi kupata maambukizi ya magonjwa hayo ni wahudumu wa afya pamoja na wazee, ndio maana wanaendesha kampeni ya kutoa chanjo.  Katika msimu wa baridi mwaka uliopita WHO ukanda wa Ulaya ilifanikiwa kutoa chanjo ya homa ya mafua makali kwa asilimia 65 ya kundi la watu walio hatarini ambao wengi ni wazee na wahudumu wa afya na msimu huu wa baridi lengo ni kuwafikia asilimia 75 ya watu hao.  Afisa wa kiufundi wa WHO Kyrgyzstan Kasymbekova Kaliya, anasema wanafahamu namna ugonjwa wa guo ulivyo hatari.…. “tunajua kwamba ugonjwa huu wa homa ya mafua makali unaweza kusababisha matatizo makubwa hasa kwa wazee wenye umri zaidi ya miaka 65, wale ambao wana magonjwa sugu ya moyo, mapafu, kisukari, na wenye hali ya uzio”.  Chanjo imeanza kutolewa kwa makundi yaliyo hatarini kuathirika zaidi ya homa ya mafua makali kama anavyoeleza Baktygul Mamatova, mtaalamu wa Kinga katika kituo cha afya cha Bishkek, “Sisi, wahudumu wa afya, kama kundi lililo hatarini ndio tumekuwa wa kwanza kupata chanjo. Siwezi sema kwamba siwezi kupata magonjwa, napata, lakini kwa kuwa nimepata chanjo ni rahisi kuhimili.”  Wazee wanfahamu umuhimu wa kupata chanjo kama anavyoeleza Kanai Alamanov, aliyefika katika  kituo cha afya cha Bishkek, “Hapo awali, kulikuwa na uhamasishaji wa kupata chanjo dhidi ya virusi vya CORONA nami nilikuja kupata chanjo hiyo ya COVID-19, na sasa ni chanjo ya homa ya mafua makali. Chanjo hii inatupa fursa ya kujikinga na magonjwa, inatupa aina fulani ya hakikisho la maisha yenye afya.”  Chanjo hazitolewi kwa wale wanaoenda hospitali pekee, wanaoishi katika nyumba maalum za kutunza wazee nao hufuatwa na kupewa chanjo kama anavyothibitisha Ludmila Kinda Ivanovna, “Mimi ninaugua sana. Mwili wangu haukubali kabisa kutumia aina nyingi ya dawa ikiwemo zile za viua vijasumu, nina pumu , nina matatizo ya moyo, nilishapata mstuko wa moyo mara mbili. Kiufupi mwili wangu ni dhaifi sana hivyo chanjo ina maana kubwa sana kwangu.”