WFP na serikali ya Madagascar zaungana mikono kubadilisha jamii za vijijini kusini mwa Madagascar kupitia mradi wa RTT
Listen now
Description
kupitia mradi wa mabadiliko ya haraka vijijini (RRT) shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP na wadau wake wameanzisha kituo maalum cha paneli za sola ambacho ni chanzo kikuu na endelevu cha maji na teknolojia ya mawasiliano ICT katika maeneo ya vijijini nchini Madagascar, hatua inayoruhusu upatikanaji wa huduma muhimu kama vile nishati, maji na mitandao ya kijamii kwa wakazi wa jamii hizo na kwa njia inayojali mazingira. Katika video ya WFP iliyopigwa na drone kutoka angani katika mkoa wa Anosy Kusini mwa Madagaska mtambo mkubwa wa paneli za sola uliojengwa na WFP na wadau unaonekana mtambo ambao ni muhimu sana kwa wana jamii wa eneo hili kwani unawasaidia kwa huduma mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji kwenye mashamba kwa ajili ya uzalishaji wa chakula.  Pia mtambo huo ni chanzo kikuu cha kusukuma maji ambayo ni huduma ya msingi na ya lazima kwa wakaazi hawa.  Ujumbe wa WFP ukiongozwa na naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Manoj Juneja umefunga safari kutoka Malagasy mji mkuu wa Madagascar hadi Anosy kushuhudia jinsi mradi huo unavyofanyakazi na kuwasaidia wananchi. Juneja anasema, “Paneli hizi za sola za mradi wa mabadiliko ya haraka vijijini zitaruhusu jamii kupata huduma ya msingi ya nishati inayojali mazingira. Na nishati hiyo inaweza kubadilishwa kwa pampu za maji, tunaweza kuchimba maji y ardhini ambayo yanaweza kutumika kunywa na kumwagilia na pia kuna fursa nyingine nyingi zinazoweza kupatikana kama ualishaji wa kilimo kupitia mafunzo, mitambo iliyopo inaweza kuruhusu pia upatikanaji wa elimu, mlo shuleni uliozalishwa hapa na mengine mengi ambayo bado hatujayafikiria”   Mradi huu unaoendeshwa na mamlaka ya mkoa unawaruhusu wadau mbalimbali kuutumia ikiwemo kuweka vituo vya mafunzo kwa ajili ya wanawake na vijana ya uzalishaji wa chakula na stadi za biashara lakini pia madarasa ya kidijitali. Madagascar ni miongoni mwa nchi 10 zilizo katika hatari kubwa ya majanga duniani na ni moja ya nchi zilizohatarini zaidi kwa vimbunga barani Afrika na mradi huu unaisaidia Anosy kujikinga na baadhi ya majanga hayo kwani takriban watu milioni 2.2 Kusini na Kusini Mashariki mwa Madagascar wanakabiliwa na kiwango cha juu cha kutokuwa na uhakika wa chakula.