Vijana wafurahia stadi za kuondokana na umaskini Sudan Kusini
Listen now
Description
Vijana katika mji wa Tambura ulioko jimbo la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini wanageuza mafunzo ya ufundi stadi kuwa nguvu ya amani na ustawi, mafunzo ambayo yalifanikishwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, UNMISS. Shamrashamra zilitawala wakati vijana 61, wakiwemo wasichana 41 na wavulana 20 walipohitimu mafunzo ya ufundi stadi yenye lengo la kuwaondoa katika umaskini na pia kuwaepusha kutumikishwa katika mzozo unaoendelea nchini humo tangu Desemba 2013. Walifundishwa urembo wa nywele, kutengeneza sabuni, halikadhalika ushoni, mafunzo yaliyofadhiliwa na UNMISS na kutolewa na shirika la kiraia Star Trust Organization, linalohusika na kupunguza ghasia kwenye jamii kwa kuwajegena vijana uwezo. Miongoni mwao ni Suzan James, mama wa watoto wawili aliyejifunza urembo wa nywele na akiwa anamhudumia mteja wakati wa mafunzo anasema. “Ninashukuru mno, kwa sababu nimejifunza mambo mengi ambayo awali sikuyafahamu, lakini sasa ninaweza kufanya. Inanisaidia sana, na ninajivunia na nina furaha. Baada ya hili, nitaenda kufungua sehemu yangu mwenyewe ya urembo wa nywele ili kusaidia jamii.” Huyu ni Justin Alex yeye amejifunza ushoni na akiwa kwenye chereheni yake anasema.. “iwapo nitapekela hii cherehani nyumbani, nitaweza kufanya kazi na kusaidia familia yangu. Kama kijana tusikae nyumbani au tusifanye uhalifu mjini na kusababisha vifo kwa jamii zetu kwa sababu si jambo zuri. Kuanzia sasa tunahitajika kushiriki kwenye shughuli za kusaidia jamii, kama kupeleka hii cherehani nyumbani ili nisaidie jamii yangu.” Wahitimu wamepatiwa vifaa vya kuanzia kufanyie kile walichojifunza. Katika hafla ya utoaji wa vyeti UNMISS iliwakilishwa na afisa wake wa masuala ya ulinzi na ujumuishaji kwenye jamii Ibrahim Tahiru ambaye amesema.. “Mradi huu unaweza kuleta amani, lakini pia mradi huu huu unahitaji amani ili uweze kuendelea. Bila amani hivi vitu vitakuwa bure. Kwa sababu wahitimu wanahitaji mazingira yenye amani ili waweze kutumia stadi zao kwa ajili ya kuboresha maisha yao na ya jamii zao. Mradi huu ni ishara ya nia yetu ya kuendelea kushirikiana na Sudan Kusini na kusaidia kufikia amani ya kudumu na kuondokana na umaskini.” Mamlaka za Tambura zina Imani kubwa na mradi huu kama asemavyo Kaimu Kamishna wa Tambura Moses Masisere. “Hakika, Tambura tumekuwa tukililia amani. Kwa hiyo kwa msaada huu tunaamini kuwa mafunzo kwa vijana zaidi kutawasaidia washiriki kwenye harakati za kiuchumi na kupunguza mauaji na uhalifu mwingine Tambura.”
More Episodes
Lengo namba 5 la Maendeleo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, ya Umoja wa Mataifa ni usawa wa kijinsia ambao ni pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fursa. Akiwa Havana Cuba hivi karibuni kwenye kongamano la kimataifa la Kiswahili Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili, alikutana na...
Published 11/26/24
Hii leo jaridani tunakletea mada kwa kina ambayo tunamskia mwanamke mjasiriamali kutoka visiwa vya Karibea St. Kitts na Neves akitumia fursa ya utamaduni wake mchanganyiko wa asili ya Visiwa hivyo na wa Kiswahili kujikwamua kiuchumi kupitia ubunifu wa mitindo na shughuli za mama lishe. Pia...
Published 11/26/24