UNESCO: Tunapaswa kuthamini sauti za walimu kote duniani
Listen now
Description
Washiriki wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walimu ililofanyika leo Oktoba 4 katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) jijini Paris, Ufaransa  wamesisitiza wito wa kuthamini mawazo ya walimu katika kuboresha elimu ya ulimwengu.  Kama tunavyofahamu, siku yenyewe ya Kimataifa ya Walimu ni kesho Oktoba 5 kama ilivyo ada ya kila mwaka lakini katika makao makuu ya UNESCO hapa Paris Ufaransa, maadhimisho yamefanyika leo kuelekea mkesha wa siku hii muhimu kwa elimu ya ulimwengu. Miongoni mwa waliozungumza ni Mkurugenzi Msaidizi Mkuu wa Elimu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Bi Stefania Giannini, ambaye ameitumia nafasi hii kusisitiza kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni 'Kutambua sauti za walimu.' Anasema, “walimu ni uti wa mgongo wa mifumo ya elimu na mawakala wakuu wa mabadiliko ya kubuni sera za elimu na kufanikisha SDGs. Tunapaswa kuthamini sauti za walimu; hili ndilo lengo kuu la Siku ya Kimataifa ya Walimu mwaka huu.” Kulingana na takwimu zilizotolewa na UNESCO, dunia inahitaji walimu wa ziada milioni 44 ili kufikia elimu ya msingi na sekondari kwa wote ifikapo mwaka 2030. Ingawa mahitaji ya walimu ni makubwa zaidi katika baadhi ya maeneo, uhaba wa walimu ni wa kimataifa. Walimu wanajiondoa kwenye taaluma hii kwa kiwango mara mbili zaidi ya miaka mitano iliyopita, hasa katika elimu ya sekondari. Hii inatokana na hali zao za kazi, zikiwemo mishahara midogo, mzigo mkubwa wa kazi, na ukosefu wa ushiriki katika maamuzi yanayohusu elimu. Akiiangizia changamoto hii, Mkurugenzi wa Kimataifa wa Elimu na Maendeleo ya Vijana katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Bi. Pia Britto, aliyejiunga katika hafla ya leo kwa njia ya video akiwa Pakistani amesema, "Leo nilikuwa na fursa nzuri ya kuzungumza na walimu wengi, ikiwa ni pamoja na mwalimu Tahseen Bashir hapa Islamabad, ambaye amenieleza baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ikiwa ni pamoja na kufundisha madarasa mengi, uhaba wa vifaa vya kujifunzia, na changamoto za kutoweza kufundisha namna wanavyodhamiria. Lakini pia amenieleza jinsi alivyofurahi kuona wanafunzi wake wakifaulu. Wakati sauti ya mwalimu inaposikilizwa na wakati sauti za walimu zinapopewa kipaumbele, wanajiona kama wadau katika kuboresha elimu kwa wakati wote, na hatua hizo zinahitajika ili kuleta mabadiliko chanya hasa katika hali ngumu zaidi." Siku hii ya kimataifa ya walimu ni mahususi kwa ajili ya kutambua na kusherehekea mchango muhimu wa walimu ulimwenguni kote katika kutoa elimu bora na kujenga mustakabali wa jamii. Pia, ni fursa ya kuangazia changamoto wanazokabiliana nazo walimu. Kutoka hapa Paris Ufaransa, mimi ni Cecily Kariuki..
More Episodes
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hususan jimboni Kivu Kaskazini kwenye mji mkuu, Goma, Alhamisi ya Oktoba 3 iligubikwa na kiza nyakati za asubuhi baada ya boti kuzama kwenye Ziwa Kivu. Ilikuwa inasafiri kutoka Minova, jimboni Kivu Kusini. Zahma hii imesababisha vifo kwa mujibu wa...
Published 10/04/24
Hii leo jaridani tunaangazia machafuko nchini Lebanon, na kesho ikiwa ni Siku ya walimu Dunia tunakupeleka Paris, Ufaranza kutsikia toka UNESCO. Makala tunafuatili ajali ya boti iliyozama katika ziwa Kivu nchini DRC na mashinani tunakupeleka Burundi, kulikoni?  Mashirikika ya kibinadamu ya Umoja...
Published 10/04/24