JAJI MKUU WA IRAN AMESEMA HAWATIKISWI NA VILIO KUHUSU ADHABU YA KIFO KWA WAANDAMANAJI.
Description
Jaji mkuu wa Iran Ebrahim Rais amefifisha matumaini kwamba adhabu ya kifo iliyotolewa kwa waandamanaji watatu vijana wa kiiran itafutwa kufuatia malalamiko ya mitandaoni.
Jaji mkuu huyo amesema maandamano yanakubalika lakini machafuko na fujo vinavyohatarisha usalama wa taifa ni mstari mwekundu.
Ameongeza katika matamshi yaliyochapishwa na shirika la habari Isna, kwamba katika matukio kama hayo mahakama haiwezi kushawishiwa na kampeni na propaganda.
Chini ya hashtag ya kupinga hukumu hiyo ya No ToExecution, mamillioni ya raia wa Iran wametumia Mitandao ya kijamii kupinga hukumu baada ya mahakama ya juu kuthibitisha adhabu ya kifo iliyotolewa dhidi ya Amirhossein M, Mohammad R, na Saeed T.
Msemaji wa wizara ya sheria ya Iran Gholam Hussein Ismail amesema wanaume hao waliongoza magenge ya vurugu na walijirekodi video wakichoma moto majengo kadha na miundombinu ya usafiri wakati wa maandamano ya Novemba, mwaka 2019.
Novemba mwaka jana,Iran ilitikiswa na maandamano ya siku kadhaa yaliyochochewa na kupanda kwa bei ya mafuta. Hata hivyo, maandamano hayo yalizimwa na vikosi vya usalama.