RAIS GHANI WA AFGHANISTAN KUWAACHIA WAFUNGWA HATARI WA KUNDI LA TALIBAN.
Description
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amesema atatoa amri ya kuachiwa huru kwa wafungwa 400 wa kundi la wanamgambo wa Taliban baada ya baraza la jadi la viongozi wa kikabila kuunga mkono hatua hiyo kama njia ya kufufua mazungumzo ya amani.
Akizungumza wakati wa hotuba yake ya kufunga mkutano wa baraza hilo linalojulikana kama 'loya jirga' amesema atatia saini amri hiyo kama ilivyotakiwa na kundi la Taliban na baada ya viongozi hao wa kikabila kufikia mwafaka.
Uamuzi huo utaondoa kikwazo cha mwisho kilichotatiza kusonga mbele kwa mazungumzo ya kusaka amani kati ya serikali mjini Kabul na kundi la Taliban. Ghani alilazimika kuitisha kikao cha baraza hilo baada ya kushindwa kutoa idhini ya kuachiwa wafungwa hao 400 ambao wengi wanatuhumiwa kwa makosa makubwa ya jinai ikiwemo kupanga mashambulizi yaliyowaua maelfu ya raia Afghanistan na wageni.
Vilevile Serikali ya Afghanistan na kundi la wanamgambo la Taliban wanakaribia kuafikiana kuhusu mazungumzo ya amani baada ya wawakilishi wa makabila kuidhinisha kuachwa huru wafungwa 400 waliokitovu cha mvutano kati ya pande mbili.
Azimio hilo limefikia mwishoni mwa mkutano wa siku tatu unaofahamika kama 'loya jirga' unaowakutanisha viongozi wa kikabila na wawakilishi wa makundi mengine, mkutano ambao wakati mwingine huitishwa ili kutafuta majibu ya masuala tata.
Mjumbe mmoja wa mkutano huo amesema kwa lengo la kuondoa vizingiti vya kuanza kwa mazungumzo ya amani na kukomesha umwagaji damu, baraza hilo limeridhia kuachiwa huru kwa wafungwa 400 kama kundi la Taliban lilivyotaka.
Orodha ya wafungwa hao inajumuisha wale wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa ya jinai ikiwemo kushiriki kwenye mashambulizi yaliyowaua maelfu ya raia wa Afghanistan na wageni.