FAIDA 8 ZA KUWEKA AKIBA UNAZOPASWA KUZIFAHAMU.
Description
1. Uhuru wa kifedha.
Uhuru wa kifedha ni zaidi ya kuwa na fedha, uhuru wa kifedha ni kuwa mtu ambaye unatakiwa kuwa maishani na kuweza kufanya au kupata kile unachokihitaji maishani.
Hata hivyo pesa ni muhimu sana kwenye suala la uhuru wa kifedha,ingawa pesa hizi zinatakiwa ziambatane na fikra sahihi.
Kwa njia ya kujiwekea akiba utaweza kujijengea msingi mzuri wa kifedha ambao ukiambatanishwa na fikra sahihi utakuletea uhuru wa kifedha.
2. Matumizi mazuri ya pesa.
Kama nilivyoeleza hapo mwanzo kuwa kuweka akiba sio kuwa na pesa nyingi bali ni maamuzi na mipango stahiki pekee.
Hivyo kuweka akiba kutakufaidisha kwa kukuwezesha kutumia pesa vyema.ikiwa unapata elfu 10 kwa siku,itakubidi uitumie vizuri ili uweze kutenga pesa ya akiba.
Kama huweki akiba huna haja ya kutumia pesa vyema kwani hakuna sehemu ya akiba inayotakiwa kutengwa.
3. Kujiandaa kwa dharura
Watu wengi huingia kwenye madeni au kupata uhitaji mkubwa wa pesa mara wapatwapo na dharura. Hivyo kwa kuweka akiba utapata faida ya kukuepushia mahangaiko wakati wa dharura kama vile magonjwa, misiba majanga n.k
4. Kuweza kufanya manunuzi au miradi ya gharama kubwa
Kuna manunuzi au miradi inahitaji pesa nyingi ili kuitekeleza. Maswala kama vile ujenzi wa nyumba, ununuzi wa viwanja kununua gari n.k, ni baadhi ya mambo yanayohitaji fedha nyingi.
Hivyo,kwa kuwa na akiba utaweza kutekeleza mambo haya kwa urahisi kuliko ungeyafanya bila akiba.
5. Kuweza kumudu wanaokutegemea
Ikiwa kuna watu wanaokutegemea kama vile wazazi, ndugu au watoto ni vyema kuweka akiba ili uwe na fedha ya kukidhi mahitaji yao mara wapatwapo na uhitaji.
Kutokuweka akiba kutakufanya uhangaike huku na huko ili kutafuta pesa ya kukidhi mahitaji ya wategemezi wako kama vile chakula, matibabu au hata ada za shule.
6. Utulivu wa akili
Unapokuwa huna akiba yoyote huwezi kuwa na utulivu wa akili, Kila wakati unahofu na wasiwasi juu ya maisha yako, unajiuliza likitokea tatizo itakuwaje? au hitaji fulani linalokuja hivi karibuni itakuwaje?n.k
Unapokuwa na fungu fulani la akiba huna haja ya kuwa na wasiwasi kwa unajua hata ukikosa pesa akiba yako itakusaidia.
7. Hukuwezesha kuandaa kesho vyema
Maandalizi ya kesho yanafanywa leo.kuweka akiba maana yake unajiandaa na mahitaji ya kifedha ya baadaye yaani kesho.mtu asiye kuwa na akiba mara nyingi hafikirii Kuhusu kesho wala hamna malengo kwa ajili ya baadaye yake.
Ili kujenga baadae au kesho njema,ni muhimu pia kuimarisha msingi wako wa kiuchumi kwa njia ya kuweka akiba.
8. Hukuwezesha kuwahi fursa
Ni mara ngapi umekuwa ukisema au ukisikia kauli kama vile" ningekuwa na pesa ningenunua hiki kitu",au "ningekuwa na pesa ningejiunga kwenye hii huduma" au "ningekuwa na pesa ningejiunga kwenye huu mradi".n.k
Hili kinadhihirisha watu hukosa fursa mbalimbali kutokana na kukosa akiba ya pesa,unapokuwa na akiba ya pesa ni rahisi kuwahi fursa mpya au bidhaa zenye manufaa mara zinapopatikana.
Hitimisho
Fedha ni jambo linalohitaji nidhamu na busara ya hali ya juu, vivyo hivyo kuweka akiba ni swala linalohitaji kufanya maamuzi sahihi ili uweze kulitekeleza.