IRAN : YATISHIA KUCHUKUA HATUA KAMA MARUFUKU YA SILAHA ITAREFUSHWA.
Description
Rais wa Iran Hassan Rouhani ametishia kuwepo na madhara iwapo baraza la usalama la umoja wa Mataifa litarefusha marufuku ya silaha dhidi ya Iran kwa shinikizo la Marekani.
Rouhani amesema kupitia televisheni ya taifa, kwamba azimio nambari 2231 la umoja wa Mataifa, ambalo ni sehemu ya makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa mjini Vienna mwaka 2015 linahitaji marufuku hiyo iondolewe ifikapo mwezi Oktoba.
"Hivi sasa wamarekani wamependekeza azimio dhidi ya sehemu ya azimio nambari 2231 ili kulikiuka. Tuna matumaini makubwa kwamba Marekani itashindwa. Tuna matumaini makubwa tena, kwamba Marekani itagundua kushindwa kwake na kushuhudia kutengwa kwake, amesema Rouhani.
Marekani ilijitoa kwenye makubaliano hayo mei 2018,na baadae utawala wa Trump ukaiwekea Iran vikwazo zaidi.
Makubaliano hayo yamekabiliwa na kitisho cha kuvunjika, kwa sababu Mataifa yaliyosalia China, Ufaransa, Uingereza, Urusi na Ujerumani, hayawezi kutekeleza sehemu ya kiuchumi ya makubaliano kukiwa na vikwazo vya Marekani,hali iliyoisukuma Terhan pia kuanza kuyakiuka.