Nadipo: Asante WFP kwa mradi wa mizinga ya nyuki sasa familia yangu inatabasamu
Listen now
Description
Kaunti ya Turkana Kaskazini mwa Kenya moja ya maeneo kame mradi wa ufugaji nyuki wa WFP umekuwa mkombozi kwa wakulima walioathirika na mabadiliko ya tabianchi. Katika kaunti hii vumbi linalotimuka katika eneo tambarare lisilo na miti linakufanya kujiuliza je Nini kizuri kinaweza kufanyika hapa kwenye ukame uliotamalaki? Lakini cha kustaajabisha ni kwamba kwa kuwezeshwa mengi yanawezekana ikiwemo njia bora za kuhakikisha uhakika wa chakula na hata kubadili maisha ya watu kama anavyosema mkulima wa nyuki Nadipo Lotelei mnufaika wa mradi wa mizinga ya nyuki kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP. “Hatua iliyochukuliwa na WFP kutupatia mizinga ya nyuki imekuja kama nyota ya jaha kwangu kwa sababu  siwezi kutembea umbali mrefu kutokana na ajali niliyopata. Mradi huu umenisaidia sana mimi ili kuweza kusaidia watoto wangu na mke wangu. Mke wangu ameweza kuanzisha biashara ya duka kutokana na faida niliyopata ambayo sasa inatumika kama chnzo cha kipato cha mahitaji ya kaya yetu.”Nadipo ni miongoni mwa wafuga nyuki 1,900 katika kaunti ya Turkana ambao wamepewa mafunzo ya ufugaji nyuki na vifaa kupitia mradi wa WFP kwa ushirikiano na shirika binafsi la HIVE ambalo mwenyekiti mtendaji wake ni Christopher Nzuki. “Tunahusika katika ufungaji na usambazaji wa vifaa. Na wakati huohuo tunatoa mafunzo kwa wafugaji nyuki na kisha kuwapatia masoko. Tunachukua kila kitu wanachozalisha.”Ufugaji wa nyuki wa kisasa si kazi kubwa, na pia unatumia nafasi ndogo na maji kidogo. Nyuki huchavusha asilimia 80 ya miti ya maua ikiwemo mazao ya chakula. Huzalisha asali, nta, mafuta na sumu, bidhaa ambazo huuzwa kwa gharama kubwa sokoni. Kwa sasa WFP inasaidia karibu wafugaji wa nyuki 5,000 katika kaunti 9 nchini Kenya lakini lengo ni kuwafikia wengi zaidi na mradi huu kama anavyosema afisa wa WFP Timothy Koskei. “Dhamira yetu mwisho wa yote ni kuwafikia wastani wa wafuga nyuki 10,000 katika kaunti 9 na kuvuna takriban tani 600 za asali.” Kwa mujibu wa WFP nyuki wana uwezo mkubwa na wanaweza kutoa mavuno mengi ambayo ni neema kwa familia sisizojiweza katika maeneo haya kame. Mkurugenzi wa WFP nchini Kenya Lauren Landis anasema mradi umezaa matunda. “Hivi sasa tunasikia kutoka miongoni mwa wanaufaika ambao awali walikuwa wakipokea msaada wa chakula ,ambao sasa sio tu wanazalisha asali  kwa ajili ya faida bali pia wanafikiria kuongeza ununuzi wa pembejeo zaidi kutoka kwa Hive. Hivyo tunachokishuhudia ni mchakato ulio wazi ambapo mtu anatoka kuwa mpokea msaada na kuwa mteja, kuwa mpokeaji wa faida na si mpokeaji wa msaada wa chakula.”Kwa mafanikio haya WFP inasema itaendelea kupanua wigo wa mradi huu ili kunufaisha familia nyingi zaidi.
More Episodes
Kila siku, mamilioni ya watoto kote ulimwenguni huenda shule wakiwa na njaa, wengi wao wakiteseka na utapiamlo sugu ambao huathiri ukuaji wa kiakili na utendaji wao katika masomo. Wanaobahatika huweza tu kumaliza masomo yao na kufanikiwa maishani kutokana na programu ya ‘mlo ya...
Published 10/21/24
Hii leo jaridani tunaangazia mkutano wa COP16 katika mji wa Santiago de Cali au Cali huko nchini Colombia na ufugaji nyuki Turakana nchini Kenya. Pia tunakupeleka nchini Somalia kufutilia programu wa WFP wa mlo shuleni na mashinani inatupeleka nchini Lebanon. Mkutano wa 16 wa nchi wanachama wa...
Published 10/21/24