Kuelekea miezi 6 ya mzozo wa Gaza, Guterres apinga matumizi ya akili mnemba kusaka wahalifu
Listen now
Description
Kesho kutwa jumapili ikiwa ndio itatimu miezi sita ya mzozo wa Gaza, huko Mashariki ya Kati, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani akirejelea wito wake wa sitisho la mapigano kwa misinigi ya kiutu, kuachiliwa kwa mateka wote bila masharti, ulinzi wa raia na misaada ya kiutu ifikie walengwa bila vikwazo vyovyote huku akikgusia pia Israeli kutumia akili mnemba kwenye operesheni zake.  Guterres akianza hotuba yake kwa kuelezea kuwa Jumapili hii inatimu miezi sita tangu mashambulizi hayo na kuelezea kuwa tarehe 7 Oktoba ni siku ya machungu kwa Israel na dunia, kwani Umoja wa Mataifa na yeye binafsi wanaomboleza vifo vya waisrael 1,200 waliouawa hadi sasa. Hakuna kinachohalalisha mashambulizi yale ya Hamas, amesema Guterres akisema pia katika kipindi cha miezi sita pia wapalestina zaidi ya 32,000 wameuawa na wengine zaid iya 75,000 wamejeruhiwa. Maisha ya watu yametwamishwa na heshima ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu imesambaratishwa. Akarejelea ziara yake ya hivi karibuni kwenye kivuko cha Rafah ambako anasema nilikutana na wasaidizi wa kiutu wabobezi walionieleza wazi kuwa janga hili na machungu ya Gaza si ya kawaida na hawajawahi kushuhudia kokote. Na zaidi ya yote anasema aliona misururu mirefu ya malori yenye shehena za misaada yakiwa yamezuiwa kuingia Gaza. Anasema pindi milango ya misaada inapofungwa, milango ya njaa inafunguliwa. Zaidi ya watu milioni moja wanakabiliwa na njaa. Watoto hivi sasa wanakuga kwa njaa na kukosa maji. Hakuna kinachohalalisha adhabu hii ya jumla kwa wananchi wa Palestina. Ameelezea pia kuchukizwa na kitendo cha Israel kutumia Akili Mnemba kusaka wahalifu Gaza tena kwenye maeneo yenye watu wengi. Akili Mnemba inapaswa kutumika kwa manufaa na sio kuchangia kwenye kusongesha vita. Amekumbusha kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia na waandishi wa habari nao wameuawa kwenye mzozo huo. Na zaidi ya yote. Vita dhidi ya habari imeongeza machungu.. kuficha ukweli na kurushiana lawama. Kuwanyima waandishi wa habari wa kimataifa kibali cha kuingia Gaza kunaruhusu kusambaa kwa habari potofu na za uongo. Ametamatisha hotuba yake ya dakika 7 kwa kutaka pia uchunguzi huru wa kilichotokea Gaza, utekelezaji wa kikamilifu wa azimio la wiki iliyopita la Baraza la Usalama la kutaka sitisho la mapigano na misaada ifikie walengwa kwani baa la njaa linajongea Gaza.
More Episodes
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo Dkt. Mwanahija Ali Juma, Katibu Mkuu wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua totauti ya matumizi ya maneno "ELEKEZA NA ELEZA."
Published 05/02/24
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayomulika uhuru wa vyombo vya habari ikijikita kwenye umuhimu wa uandishi wa habari na uhuru wa kujieleza katika muktadha wa kukabiliana na janga la tabianchi. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na uchambuzi wa neno la wiki. Nchini Kenya mafuriko...
Published 05/02/24