Guterres/Kwibuka 30: Vijana kemeeni kauli za chuki kokote muisikiapo na muionapo
Listen now
Description
Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu limekuwa na tukio maalum la kumbukizi ya miaka 30 ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda au KWIBUKA30, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres ametumia hotuba yake pamoja na mambo mengine kuwasihi vijana kutoka taifa hilo la Afrika Mashariki kukemea chuki kokote wanapoisikia au kuiona.  Tukio lilianza kwa ukumbi kuwa giza na video ya dakika tano ikachezwa kueleza kuwa watu wengi wanaijua Rwanda kuanzia 1994, lakini ilikuweko hata kabla ya ukoloni, na kwamba wakoloni ndio waligawa watu kwa misingi ya makundi licha ya kwamba lugha yao ilikuwa moja. Manusura na watekelezaji wa mauaji walizungumza pia kwenye video hiyo! Video ikafuatiwa na kuwasha mishumaa kukumbuka waliouawa na kisha hotuba ambapo Katibu Mkuu Guterres akawa ana ujumbe mahsusi kwa vijana wa Rwanda walioshiriki kimtandao na pia ukumbini. Anasema rafiki zangu, katu hatutasahau vitisho vya siku 100. Lakini tunahitaji msaada wenu. Tunahitaij sauti na uchechemuzi wenu kusongesha kumbukizi za wale waliouawa. Na kukemea chuki kokote muisikiako au muionapo. Mijini kwenu, vitongojini, shuleni, mtandaoni, popote pale na kila mahali. Akaendelea kusema kuwa hebu na tuondoe chuki na ukosefu wa stahmala kokote tuvionapo. Kumbukumbu za waliouawa zichochee vitendo vyetu, na azma yetu ya kuhakikisha dunia bora na salama kwa watu wote.  Guterres amesema Umoja wa Mataifa kila wakati utashikamana na vijana katika juhudi hizo muhimu.  Mauaji ya kimbari Rwanda ya mwaka 1994 yalifanyika kwa siku 100 kuanzia tarehe 7 Aprili na zaidi ya watu milioni moja waliuawa, wengi wao Watutsi, halikadhalika wahutu wenye msimamo wa kati na watu wengine waliokuwa wanapinga mauaji hayo.  Katibu Mkuu amesema siku hizo 100 ziliakisi ubaya zaidi wa ubinadamu. Lakini kipindi baada ya mauaji kilidhihirisha ubora wa roho ya ubinadamu: mnepo, maridhiano, ujasiri na nguvu.  Amesema simulizi za manusura ni ushahidi wa nguvu ya matumaini na msamaha ambapo amemtaja manusura Laurence Niyonangira ambaye alipoteza jamaa zake 37 wakati wa mauaji hayo.  “Alichagua kusamehe mmoja wa wahusika wa mauaji ya familia yake baada ya mhusika kuungama na kutumikia muda jela kwa makosa aliyotenda. Kama manusura, Laurence alisema ‘tunaweza kuponya vidonda kwa kushirikiana wale waliovisababisha.” Amesema Guterres.  Hivyo Katibu Mkuu amesema mwaka huu ambapo kumbukizi inajikita kwenye mzizi wa mauaji ya kimbari ambao ni chuki, ambayo sasa inakolezwa na mitandao ya kijamii, “ni lazima tushikamane pamoja na kurejelea shinikizo la dunia la kuridhia na kutekeleza kikamilifu Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya kimbari, huku tukiimarisha mifumo ya kuzuia, kuelimisha vizazi vipya kuhusu mauaji ya kimbari yaliyopita na kukabili taarifa potofu na za uongo ambazo huchochea kauli za chuki na nia na vitendo ya mauaji ya kimbari.” 
More Episodes
Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa mwiba kwa jamii nyingi yakizilazimu kubadili mfumo wao wa Maisha ili kukabiliana na athari zake kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa jamii zilizoathirika na janga hilo ni za watu wa asili wakiwemo Wamaasai kutoka Kenya na hususan wanawake. Je wanahimili...
Published 05/01/24
Wakati kukiwa na ongezeko la wito wa kimataifa kwa Israel kujizuia na mashambulizi zaidi Gaza na ripoti za leo za mashambulizi mengine mabaya zaidi ya usiku kucha, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kuhusu athari mbaya zinazoendelea za vita hiyo na haja ya kuhakikisha njia za...
Published 05/01/24